Tutaendelea kumuenzi Mkapa: MUM
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) umesema utaendelea kumuenzi aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Benjamini William Mkapa kwa mchango mkubwa aliotoa kwa Chuo hicho ikiwemo kutoa majengo yanayotumiwa na chuo hicho.
Hayo yamesemwa na Afisa udahili wa chuo hicho Abdulrahman Mumbu wakati Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika banda la chuo hicho lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya vyuo vikuu Mnazi mmoja jijini Dar es salaam katika siku ya kwanza ya maonesho hayo Agost 31 mwaka huu.
Mumbu amesema chuo hicho kitaendelea kukumbuka mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Mkapa ambao umechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa chuo hicho.
Afisa habari wa chuo hicho Ngaja Mchele amesema Chuo hicho kimejipanga kupokea maombi ya moja kwa moja bila malipo yoyote kwa wanafunzi watakaotembelea banda la chuo hicho na wale watakaotuma maombi yao kupitia tovuti ya chuo ambayo ni www.mum.ac.tz.
Kwa upande wa Wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu katika vyuo vikuu na vyuo vya kati wamesema Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kimeendela kuwa Chuo pekee kinachotoa Elimu bora kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Wamebainisha hayo walipotembelea banda la Chuo hicho kwa lengo la kupata ufahamu kuhusu Chuo hicho na kozi zinazotolewa ambapo baada ya kuridhishwa wamefanikiwa kufanya maombi kwa ajili ya kujiunga na chuo hicho.
Latifa Omar na Zuwena Hemedi ambao ni miongoni mwa wanafunzi waliofanikiwa kukamilisha maombi ya kujiunga na chuo hicho katika fani ya Ualimu wamesema licha ya kuwa wanapenda kuwa walimu lakini wamechagua MUM kuwa sehemu pekee itakayolinda maadili na kuwa mahili katika fani zao.