MUM, IIUM Kuanzisha Mradi wa Bidhaa Halali
Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro(MUM) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu Nchini Malaysia(IIUM) vinatarajia kuanzisha Mradi wa kutengeneza malighafi pamoja na bidhaa zinayotokana na vyanzo Halali.
Hatua hiyo inakuja kufuatia wasiwasi wa uwepo wa baadhi za bidhaa ikiwemo vipodozi na viburudishi vinavyotokana na malighafi kutoka katika vyanzo ambavyo si halali kwa mujibu wa Dini tukufu ya Kiislamu ambazo nyingi katika hizo zinatokana wanyama.
Makubaliano hayo yamekuja kufuatia kikao cha siku tatu kilichofanyika Chuoni MUM Mkoani Morogoro kuanzia tarehe 26-29 Januari, 2026 kati ya ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha IIUM Prof. Azura, Prof. Noriah na Dr. Sarina pamoja na Uongozi wa MUM ukiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Mussa Assad.
Utekelezaji wa Mradi huo utahusisha uandaaji wa eneo la ufugaji wa wanyama Halali ikiwemo Ng’ombe, ujenzi wa machinjio na viwanda vikubwa vya kuandaa malighafi kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa halali ikiwemo mifupa, pembe na ngozi huku nyama ikitumiwa katika matumizi ya kawaida ya chakula.
Katika wasilisho la kitafiti lililotolewa na ujumbe huo kutoka Chuo cha IIUM limeonesha uwepo wa matumizi ya vilainishi katika vipodozi na baadhi ya vyakula vya kuburudisha ambavyo hutokana na malighafi zitokanazo na wanyama.
Katika kufanikisha mradi huo, Prof. Assad ameongza ujumbe huo kwenye eneo la Chuo lililopo Sangasanga nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 500 kwa ajili ya utekelezaji wake.
Kufanikiwa kwa Mradi huo kutawezesha matumizi ya bidhaa zinazotokana na vyanzo halali na kutoa shaka kwa watumiaji wake.